Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ametembelea Ubalozi wa Tanzania Nchini Kenya na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Nchini humo Dkt. Pindi Chana.
Prof. Kabudi amefanya ziara hiyo wakati akihudhuria Mkutano wa 56 wa Mwaka wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya Kisheria ya Nchi za Asia na Afrika (Asian-African Legal Consultative Organisation –AALCO) unaofanyika Jijini Nairobi.
Aidha, Prof. Kabudi amempongeza Balozi Pindi Chana kwa maandalizi waliyoyafanya kuhakikisha ujumbe wa Tanzania unashiriki ipasavyo katika mkutano huo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zake zitatoa ushirikiano stahiki katika utekelezaji wa majukumu yake, na kwamba Ubalozi uwe tayari kwa kufuata taratibu zilizopo kiserikali kuwasiliana na Wizara pindi yanapoibuka masuala yanayohitaji ushiriki wa Wizara.
Kwa upande wake Balozi Dkt. Chana ameahidi kuwa ataendeleza ushirikiano mzuri na Wizara kwa kutumia taratibu zilizopo na atahakikisha kuwa masuala ya Wizara yanaifikia Wizara kwa wakati.