Waziri wa Mambo ya Nje wa Gabon, Michael Moussa Adamo (62), amefariki mjini Libreville baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri licha ya juhudi za wataalamu kujaribu kuokoa maisha yake.
Adamo ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Ali Bongo Ondimba alishiriki kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri na alianza kujisikia vibaya na kisha kukimbizwa katika hospitali ya kijeshi baada ya kupoteza fahamu.
Kufuatia msiba huo, Rais Bongo aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, “Alikuwa mwanadiplomasia mkubwa sana, mwanasiasa wa kweli. Kwangu mimi, kwanza alikuwa rafiki, mwaminifu na mkweli, ambaye siku zote niliweza kumtegemea. Ni hasara kubwa kwa Gabon.”
Michael alizaliwa Januari 10, 1961 katika mji wa Makokou na alianza kazi mwaka 1981 kama mtangazaji kwenye runinga ya taifa akiwa na shahada ya uzamili katika uhusiano wa kimataifa na mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Boston, aliteuliwa mwaka wa 2000 kuwa mkurugenzi kwenye ofisi ya Waziri wa Ulinzi.