Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema kuwa kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inashughulikia changamoto za wananchi kuanzia ngazi ya kijiji.
Akiongea na Menejimenti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI Waziri Bashungwa amesema kuwa wataalam wanatakiwa kuangalia changamoto zilizopo kwenye vijiji ili kupata picha halisi ya matatizo yanayowakabili wananchi na kupanga mipango mikakati ya kutatua kero hizo kwa jamii.
“Ninawataka watumishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi kujikita zaidi kwenye matatizo yanayojitokeza zaidi kwenye vijiji na kuyachukulia kuwa ni changamoto ya nchi nzima hivyo tunahitajika kuweka mikakati ya kuzitatua na kuwezesha wananchi katika kutoa huduma bora,”amesema Waziri Bashungwa.
Amebainisha kuwa watumishi wanapaswa kujifunza kwenye ngazi za vijiji ili changamoto wanazopata wananchi ikiwemo ukosefu wa madarasa, zahanati na mengineyo zitatuliwe haraka iwezekanavyo.
Amesema utatuzi wa changamoto hizo itasadia kutoa huduma bora kwa wananchi na kuzingatia hilo wakati wa uandaaji wa bajeti za kila mwaka kwenye wizara husika.