Polisi Nchini Afrika Kusini wamethibitisha tukio lisilo la kawaida la Waziri wa Uchukuzi, Sindisiwe Chikunga akiwa na walinzi wake kuporwa vitu kadhaa na kuibiwa silaha.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Athlenda Mathe amesema tayari wameanza msako wa kuwatafuta majambazi hao waliotoroka wakiwa na mali binafsi za watu waliokuwemo ndani ya gari hiyo na bastola mbili zanazomilikiwa na Jeshi la Polisi la Afrika Kusini – SAPS.
Aidha, taarifa ya Wizara ya Uchukuzi imesema shambulio hilo lilitokea Novemba 6, 2023 wakati Waziri huyo akiwa safirini barabara kuu iliyopo kusini mwa jiji la Johannesburg.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, “matairi ya gari la Waziri yalitobolewa na misumari, na hivyo kusababisha gari kusimama na kuwawezesha wahalifu kuwapora watu waliokuwa ndani ya gari na hakuna mtu aliyejeruhiwa.”
Hata hivyo, Polisi nchini humo wamekuwa wakirekodi matukio ya ujambazi zaidi ya 500 na mauaji 70 kwa siku katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 62, kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu (2023), kulingana na takwimu rasmi.