Waziri wa Uchukuzi wa Gabon, Brice Paillat amejiuzulu kufuatia kuzama kwa Meli ya Esther Miracle, ambayo iliua watu 21, kwa kuwasilisha barua yake kwa Rais wa Jamhuri ya nchi hiyo, Ali Bongo Ondimba ambaye amekubali ombi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari, Paillat hakubainisha sababu za kujiuzulu kwake na wala hakuzungumzia tukio la Meli hiyo kuzama, iliyokuwa ikitoka mji mkuu wa Gabon Libreville kuelekea bandari ya mafuta ya Port-Gentil Machi 9, 2023.
Katika tukio hilo, Maafisa wanne wa utawala wa Jeshi la Wanamaji na Masuala ya Baharini wamesimamishwa kazi na shughuli za mmiliki wa meli na mmiliki wa feri zimesimishwa hadi hapo itakapotangazwa vingine.
Hata hivyo, familia za waathiriwa wa ajali hiyo, wananchi, mashirika ya kiraia na wanasiasa wanasema kujiuzulu kwa Waziri wa Uchukuzi hakutoshi bali wale wote waliohusika waadhibiwe kutokana na makosa yaliyofanyika ya kutowakuongoza watu wakati wa uokoaji.