Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anakabiliwa na tuhuma mpya kuwa alikiuka kanuni za vizuizi vya maambukizi ya virusi vya corona alivyoweka nchini humo, kwa kuhudhuria sherehe ya siku yake ya kuzaliwa katika ofisi yake huku kukiwa na zuio la watu kukusanyika ndani.
Televisheni ya ITV imeripoti kuwa Johnson alihudhuria hafla hiyo iliyopangwa bila yeye kujua, mnamo Juni 19.
Zaidi ya watu 30 walihudhuria sherehe hiyo katika chumba cha mikutano ya mawaziri kwenye ofisi na makazi yake.
Kiongozi huyo wa chama cha Conservative aliyeingia madarakani 2019, anajaribu kuulinda wadhifa wake baada ya madai kuwa yeye na wafanyakazi wake walifanya sherehe ofisini kwake wakati nchi ikiwa katika kipindi kigumu cha janga la corona.
Johnson alitoa sababu kadhaa kuhusu tuhuma za awali, kwanza akisema hakukuwa na sheria zilizovunjwa na kisha akaomba radhi kwa watu wa Uingereza kwa kuonyesha unafiki kuhusu suala hilo.