Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif, amehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kutokana na kesi ya rushwa inayohusisha familia yake kumiliki mali nje ya nchi hiyo.
Mwanae wa kike Mariam Nawaz, ambaye alikuwa akionekana kuwa mrithi wake kisiasa amepatikana na hatia na kuhukumiwa miaka saba huku mumewe akihukumiwa mwaka mmoja jela.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mohammad Bashir hii leo ijumaa nchini Pakistan, ambapo imeelezwa kuwa mali ambazo anamiliki kiongozi huyo na familia yake jijini Londan nchini Uingereza zitataifishwa na serikali ya Pakstan.
Hukumu ya waziri huyo wa zamani imetolewa siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Pakstani Mnamo Julai 25.
Nawaz Sharif, ambaye ameshawahi kuwa waziri mkuu wa Pakistan kwa vipindi vitatu tofauti aliondolewa madarakani mwaka jana na mahakama kuu nchini humo kwa kukosa vigezo vya kufanya kazi kwenye ofisi ya umma kutokana na kesi ya kujilimbikizia mali iliyokuwa ikimkabili yeye pamoja na mtoto wake.