Lydia Mollel – Morogoro.
Baraza la Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF (Workers compensation fund), limetakiwa kuongeza kasi ya kuwasajili waajiri wote nchini hususani waajiri wa sekta binafsi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha sita baraza la Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi kilichofanyika Mkoani Morogoro, Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Wizara ya Kazi,Vijara naAjira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema ni vyema waongeze kasi ya kusajali waajiri nchini hasa waajiri sekta binafsi kwani ndio sekta inayoajiri wafanyakazi wengi wa ngazi ya chini na kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi.
Amesema, Bodi hiyo inatakiwa kutoa elimu kwa Umma ili wafahamu umuhimu wa mfuko huo kwani unawagusa watanzania wote kutokana na baadhi yao kupata madhara wawapo kazini, kujua namna wanavyoweza kunufaika na mfuko huo na kuwataka pia viongozi na wajumbe wa baraza hilo Kuja na mipango mipya ya namna ya kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanuafaika wa mfuko huo.
Naye Mwenyekitiwa Baraza hilo ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt John Mduma amesema watafuata maagizo yaliyotolewa na katibu mkuu kwa kuweka mikakati bora pamoja na kushirikiana na Tasisi mbalimbali zinazosajili sekta zote ili wapate waajiri na taarifa zao kwa uhakiki zaidi.
Amesema, hadi sasa baraza hilo limewasajili waajiri wasiopungua asilimia 92 na bado wanaendelea na zoezi hilo kwa kutoa elimu ya faida wa mfuko huo unaohudumia wafanyakazi waliopata madhara.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi – WCF ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 marejeo ya mwaka 2015 , inahusu waajiri na waajiriwa wote Tanzania Bara.
Pia, mfuko huo unalenga kushughulikia masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na Binafsi ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.