Uongozi na Wanachama wa Chama cha Walimu Mkoani Njombe kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutatua kero za watumishi nchini ili kuhakikisha analinda maslahi ya watumishi hao.
Akizungumza na Dar24 mwenyekiti wa CWT mkoa wa Njombe, Meckson Widzengo amesema kulingana na jitihada hizo za Rais Magufuli wanaimani kuwa Serikali itashughulikia suala la kupandishwa madaraja kwa walimu pamoja na kumaliza madeni yaliyo nje na mishahara yao.
“Nimshukuru Rais kwa kufikia muafaka kwenye suala mzima la kikokoto watumishi hasa walimu tunaenda kumpongeza na kwamba aendelee na kasi ya kutatua changamoto za walimu na watumishi kwa ujumla” amesema Widzengo.
Kwa upande wake mwakilishi wa walimu wenye ulemavu wa chama hicho mkoani Njombe Betrant Mbena, ameomba Serikali iendelee kuangalia walimu wenye ulemavu katika ugawaji wa vyeo na uongozi.
“Niiombe Serikali na waajiri wengine kuwaangalia sana walemavu katoka masuala mbalimbali ikiwemo la ugawaji wa vyeo pia walemavu wajiandae ili kustaafu vizuri” amesema Mbena.
Uongozi wa CWT mkoa wa Njombe wanaunga mkono mpango wa serikali wa kuweka leseni za kufundishia kwa walimu kwani itaongeza ufanisi kwa walimu.