Msanii wa Maigizo, Wema Sepetu amekihama rasmi Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema.
Amesema sababu kubwa ya kuhamia CHADEMA ni kutafuta nafasi ya kupigania demokrasia anayodai kuwa inapotea kila kukicha nchini Tanzania.
Aidha, Sababu nyingine aliyoieleza Wema ni kutelekezwa na CCM licha ya kujitolea kutoa mchango wake kwa chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kiasi cha kuwa kuhatarisha maisha yake na kutishiwa kumwagiwa tindikali visiwani Zanzibar.
“Kuanzia sasa mimi siyo tena mwanachama wa CCM, na muda mfupi ujao nitachukua kadi yangu ya Chadema nimeamua kuingia Chadema kwa sababu nataka kupigania demokrasia, laiti ningejua ningeingia zamani sana, najua nimewahi kusema kuwa nitakufa nikiwa CCM, lakini sikujua kama itakuwa hivi, amesema Wema.
Hata hivyo, mesisitiza kuwa hajahamia CHADEMA kwa sababu ya pesa kama ambavo imekuwa ikidaiwa, bali ni kwa ajili ya kupigania demokrasia, na kuweka wazi kuwa kuanzia sasa ameingia kwenye mapambano ya kupigania demokrasia akiwa kwenye chama ambacho anaamini kuwa ni chama pekee chenye uwezo wa kurejesha demokrasia inayopotea.
Wema pia amesema kuwa kuna baadhi ya wasanii wanaidai CCM ambapo amesema kuna madeni mengi ambayo wanadai lakini wamekuwa wakizungushwa na kuambiwa wakamdai JK.