Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger ameitabiria makubwa klabu hiyo kuelekea msimu ujao 2023/24, kwa kusema ina nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.
Mzee huyo ameweka neno pia juu ya usajili wa pesa nyingi uliofanywa na Arsenal baada ya kukubali kulipa Pauni 105 milioni kunasa saini ya kiungo Declan Rice kutoka West Ham United.
Wenger mwenye umri wa miaka 73, alidumu kwenye kikosi cha Arsenal kwa muda mrefu baada ya kuanza kukinoa mwaka 1996 hadi 2018. Katika muda wake, Mfaransa huyo alishinda Ligi Kuu England mara tatu na Kombe la FA mara saba.
Kwa sasa Wenger ni bosi wa FIFA kwenye upande wa maendeleo ya soka. Taji lake la mwisho la Ligi Kuu England lilikuwa 2004 ndilo la mwisho kubebwa na Arsenal, haijachukua tena tangu muda huo.
Mchezaji wake wa zamani, Mikel Arteta ambaye kwa sasa ndiye kocha wa Arsenal alikaribia kuhitimisha miaka 18 ya ukame wa taji la Ligi Kuu England wakati miamba hiyo ilipoongoza ligi kwa muda mrefu msimu uliopita kabla ya kupigwa kikumbo na Manchester City iliyonyakua ubingwa.
Arsenal ilipoteza uongozi wake wa pointi nane kileleni na kuwaachia Man City wakinyakua taji hilo la Ligi Kuu England kwa mara ya tatu mfululizo.
Arteta sasa amepania kufanya kweli msimu ujao baada ya kunasa mastaa Rice, Kai Havertz na Jurrien Timber.
Na baada ya usajili wa pesa nyingi wa Rice, Wenger alisema Arsenal sasa inaweza kwenda hatua moja juu zaidi na kushinda taji la Ligi Kuu England msimu ujao.
Wenger alisema: “Naamini tutashinda ubingwa, ni rahisi tu kama hivyo. Rice? Nadhani ni uwekezaji mzuri. Nadhani Arsenal imefanya usajili mzuri, bado vijana, hivyo watacheza pamoja kwa miaka mingi. Watakuwa kwenye presha kubwa baada ya mwaka jana, lakini wanaweza kujifunza kutokana na makosa na kufanya kweli safari hii.
“Mimi nilipambana kipindi kile hakuna pesa, lakini Arsenal kwa sasa ipo vizuri kifedha na wanafanya usajili wanaodhani unatosha kuwapa ubingwa.”