Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amepanga kuwatumia kwa zamu makipa wa klabu hiyo Petr Cech pamoja na David Ospina licha ya kuonekana mambo yalikua mabaya wakati wa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya usiku wa kuamkia jana huko mjini Zagreb nchini Croatia.

Mlinda mlango kutoka nchini Colombia, David Ospina, alipewa jukumu la kukaa langoni wakati wa mchezo huo ambao ulimalizika kwa Arsenal kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Dynamo Zagreb, hali ambayo ilizusha maswali mengi kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa kuhoji kwa nini Arsene Wenger asingemchezesha Petr Cech.

Wenger alijitetea kufanya maamuzi hayo kwa kusema hakuona tofauti ya kumtumia Ospina katika mchezo huo kutokana na uwezo alionao huku lengo lake kubwa lilikua ni kutaka kumpumzisha Petr Cech ambaye ameonekana langoni tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Wenger, aliwaambia waandishi wa habari kwamba wawili hao wana uwezo unaotaka kushabihiana na atakua mwendawazimu kuendelea kumtumia mlinda mlango mmoja katika kila mchezo, utakaokihusu kikosi chake kwa msimu huu.

Mzee huyo kutoka nchini Ufaransa, aliwakumbusha waliohoji kwa nini alifanya maamuzi ya kutomtumia Petr Cech katika mchezo wa juzi, kwa kusema Ospina alikuwepo klabuni hapo msimu uliopita na alionyesha uwezo mkubwa mpaka wakafanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Hata hivyo akasisitiza kwamba kila mchezaji kwenye kikosi chake anastahili kucheza kutokana na mchezo unaowakabili kwa msimu huu, na kufungwa katika mpambano wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Dynamo Zagreb sio kipimo cha kumnyoshea kidole yoyote kwa kumtuhumu kupitia kigezo cha uzembe.

Ospina alijiunga na Arsenal mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea nchini Ufaransa alipokua akiitimikia klabu ya Nice na Petr Cech amekua mchezaji pekee aliyesajiliwa huko Emirates kwa msimu huu akitokea Chelsea.

Ligu Kuu Bara Katika Mzunguuko Wa Tatu
Kipyenga Cha FDL 2015-16 Kupulizwa Kesho