Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amewaonya wachezaji wake kwa kuwataka kuwa makini wanapocheza michezo yote ya ligi ya nchini England pamoja na michuano mingine wanayoshiriki msimu huu.

Wenger, waliwasilisha onyo hilo kwa wachezaji wake mara baada ya ushindi wa mabao matatu kwa sifuri waliouvuna kutoka kwa Man Utd, ambao walikua wageni kwenye uwanja wa Emirates jana jioni kwa saa za Afrika mashariki.

Wenger amewataka wachezaji wake kutobweteka na ushindi huo na badala yake wauchukulie kama changamoto ya kujituma kila kukicha huku wakiamini hakuna linaloshindikana pale wanapoamua kujituma.

Amesema ushindi walioupata kwa Man Utd ulitokana na kujituma kwa kila mchezaji wake, sambamba na kuhimizana walipokua uwanjani, hali ambayo anaamini ikiendelezwa kwenye michezo yote watakayocheza msimu huu kutakua na matarajio chanya wanayoyategemea.

Mzee huyo kutoka nchini Ufaransa, amesema lilikua kusudio lao kupata matokeo mazuri na walijipanga kufunga mapema kwa kuamini wapinzani wao wangechanganyikia, hali ambayo ilitokea na hatimae kufikia lengo la kukusanya point tatu muhimu nyumbani.

Katika hatua nyingine Arsene Wenger amewasisitiza mashabiki kuendelea kuwa sambamba na kikosi chao, kwa kuwataka kukubaliana na hali yoyote ya kimchezo.

Kibopa Wa Mbeya City Atoa Tamko Dhidi Ya Nyosso
Mourinho: Nitaondoka Wachezaji Wakinikataa