Leo ni siku ya maadhimisho ya kupambana na UKIMWI Duniani, ambapo Shirika la Afya Duniani, WHO na ofisi ya shirika hilo katika Umoja wa Ulaya wamesema bila ya vipimo, watu wengi wamekuwa wakiishi na virusi vya UKIMWI barani Ulaya, na hawagunduliki.
WHO inasema, kutokana na hali kama hiyo kwa mwaka 2021 pekee watu 300 waligundulika kuwa na virusi vya ukimwi VVU, kila siku katika nchi 46 kati ya 53 za Ulaya ambazo zilifanyiwa tahmini na wataalamu wa masuala ya afya.
Ripoti hiyo, pia inaonesha kuwa bado kuna unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, VVU na kwamba suala hilo linapaswa kuangaziwa kwa ukubwa ili kunusuru maisha ya watu na kudhibiti maambukizi.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO barani Ulaya, Hans Kluge amesema kutokana na takwimu za upimaji wa VVU, matibabu na huduma upo uwezekano wa ugonjwa huo kuendelea kuenea na uwepo wa unyanyapaa dhidi ya VVU kunaleta uoga wa watu kupima.