Jumla ya watu watano wamefariki kwenye maandamano ya vurugu zinayoendelea kuhusu kuondolewa kwa rais wa zamani Pedro Castillo madarakani, nchini Peru.
Hatua hiyo inajiri licha ya juhudi za Rais mpya kujaribu kuyatuliza maandamano hayo ambapo hadi sasa jumla ya watu saba wakiwemo vijana watatu wameuawa tangu Pedro Castillo wa siasa za mrengo wa shoto alipotuhumiwa kwa jaribio la mapinduzi.
Mnamo Jumapili, rais mpya Dina Boluarte alijaribu kutuliza vurugu kwa kutangaza kuwa ataitisha uchaguzi miaka miwili ijayo, na alitangaza hali ya tahadhari katika maeneo yenye machafuko.
Hapo jana, takriban waandamanaji 2,000 waliziba barabara, kuwasha moto barabarani na kulazimisha uwanja wa ndege ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo kusitisha shughuli zake kwa saa kadhaa.