Pamoja na kutangaza wachezaji watatu mpaka sasa, klabu ya Simba SC imesema bado haijamaliza zoezi la usajili, huku ikitangaza nafasi tatu hadi nne ambazo inatarajia kushusha ‘vyuma’ vipya vya kimataifa kabla ya dirisha kufungwa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema mpaka sasa walichofanya ni kama dibaji tu, lakini bado hawajamaliza usajili kwani tangu mwanzo waliahidi kuwa wanafanya maboresho makubwa kwenye kikosi hicho na kazi ndiyo kwanza imeanza.
“Hiyo ilikuwa ni dibaji tu bado hatujamaliza usajili, kumbuka tunafanya maboresho ya kikosi chetu, kama ni gari basi tunafanya kazi ya kushusha injini tunaweka mpya, kubadilisha matairi tunaweka mapya, kupiga bodi rangi, tunabadilisha viti, tunasafisha ili kuitengeneza Simba mpya na iliyokuwa imara.
“Kuna nafasi tatu au nne hivi zimebaki, bado kiungo mkabaji tunae ila hatujamtambulisha, winga teleza ya kuingia na kufunga na pia bado golikipa na mwingine hivi, kwa hiyo wanachama na mashabiki wa Simba SC wakae kwa kutulia, mambo bado,” ametamba Ahmed.
Akizungumzia usajili wa Che Malone, amesema wamempa mkataba wa miaka mitatu, na ndiye mchezaji ambaye aliwapa tabu sana kupata saini yake kwa sababu walikuwa wanamgombea na klabu mbalimbali za Afrika na bara la Ulaya.
“Che Malone amekuwa mnyama kwa mkataba wa miaka mitatu, kulikuwa timu nyingi zilikuwa zinamhitaji, watu wakipanda dau, zipo za Afrika na za Ulaya Mashariki, Austria, Sweden na Uswisi zilikuwa zinamtolea macho.
“Kwa mchezaji kama huyu umri wa miaka 24 anachezea Taifa la Cameroon, unajua wachezaji wa Afrika Magharibi wanaaminika sana huko kwa sababu kuna watu wameshatangulia sokoni na wamefanya vizuri, kwa hiyo alikuwa anawindwa sana, Simba tukanyang’anyana nao na kufanikiwa kumpata na siku zote mwenye kisu kikali ndiye aliyekula nyama,” amesema.
Kuhusu utambulisho wa wachezaji wengine amesema bado alikuwa hajapata mrejesho kutoka kwa viongozi wake, lakini huenda juma hili wakamtangaza mchezaji mwingine, hata hivyo jana klabu hiyo ilitangaza kumwongezea beki wa kulia, Shomari Kapombe mkataba wa miaka miwili zaidi ambapo sasa ataitumikia Simba SC hadi mwaka 2025.
Wakati huo huo kikosi cha Simba SC kimeondoka leo Jumanne (Julai 12) kuelekea Uturuki kwa kambi ya wiki tatu, huku nyota wao mpya, Che Malone, akionesha kufurahishwa na mapokezi mazuri aliyoyapata, hivyo kuahidi kufanya kile kilichosababisha asajiliwe kwa kuwarudishia furaha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo.
“Kwa sasa ni mchezaji wa Simba SC, naahidi nitafanya kazi ya kuwapa furaha wapenzi wa klabu hii kubwa, kwani wamenipa mapokezi mazuri sana,” amesema beki huyo wa kati aliyesajiliwa kutoka Cotton Sport ya Cameroon.