Mbunge wa Nyamagana anayemaliza muda wake, Ezekiel Wenje amewataka wanachama wa Chadema kutokuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa.

Akiwahutubia wanachama wa chama hicho jijini mwanza hivi karibuni, Wenje aliwahakikishia wanachama wa chama hicho kuwa Dk. Slaa bado ni mwanachama wa chama na kwamba atajiunga na kampeni hivi punde.

“Kuna vitu vichache ambavyo Katibu Mkuu wetu, Dk. Wilbroad Slaa bado ana mashaka nayo na ndio sababu chama kimempa nafasi ya mapumziko. Lakini nawahakikishia kuwa Dk. Slaa hajakiacha chama. Bado yuko Chadema na atajiunga nasi kwenye kampeni hivi punde,” Wenje alisema.

Akiongelea uamuzi wa chama hicho kumkaribisha Edward Lowassa, Wenje alisema kuwa wajumbe walimhoji Edward Lowassa na kujiridhisha kuwa hakuhusika na ufisadi wa Richmond.

“Lowassa alituhakikishia kuwa hahusiki kabisa na sakata hilo. Alituhakikishia kuwa hakuna uthibitisho wowote kwamba yeye alihusika na ufisadi wa Richmond. Tulimuuliza maswali mengi na aliweza kutushawishi kwamba hahusiki kabisa na ufisadi wa Richmond,” Aliongeza.

Dk. Slaa ni mmoja kati ya wanachama wa Chadema ambao hawakukubaliana na ujio wa Edward Lowassa Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais huku kumbukumbu zikionesha kuwa chama hicho kilimtuhumu kwa maneno makali kuwa yeye ni fisadi na alihusika na kashfa ya Richmond mwaka 2008, sakata lililosababisha ajiuzulu uwaziri mkuu.

Valbuena Akubali Kurejea Nyumbani
FA: Kadi Nyekundu Ya Courtois Ilistahili