Serikali imewasilisha pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wanaochukua Stashahada katika vipaumbele vya kitaifa, kupewa mikopo ili kuwawezesha kuchukua elimu husika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,amesema mabadiliko hayo, yanalenga kuwezesha kasi katika uchumi wa viwanda.
Aidha, Ndalichako amesema mabadiliko katika Sheria Namba 4 ya Mwaka 2016 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), yamelenga kutoa nafasi ya Kada ya Stashahada inayohitajika ambao wamekuwa hawapati mikopo.
“Kwa lengo la kupata usawa na kwa kuwa Diploma nayo iko kwenye Elimu ya Juu, watoto ni wale wale,kuna wengine nao wanashindwa kumudu gharama na ili Serikali ipate uwiano mzuri tumeona ni vizuri kuwe na marekebisho ya sheria,”amesema Profesa Ndalichako.
Hata hivyo, Ndalichako amesema kuna umuhimu mkubwa wa Kada ya Stashahada, hasa wanaokwenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa kwenye msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa Ujenzi wa Taifa la Vijana, kama ilivyo kwa wenye Shahada.
Hata hivyo, HESLB imesema kuwa maamuzi ya kusitisha utoaji wa mikopo, ulilenga kutekeleza maagizo ya Serikali, ambapo, Ndalichako amesema kwamba uamuzi wa kusimamisha mikopo hiyo, ulitokana na nia ya Serikali kufanya mabadiliko katika sheria hiyo ili kuipa wigo mpana zaidi kuliko kujikita katika eneo la Sayansi pekee.