Mratibu wa miradi ya Benki ya Dunia, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Humphrey Kanyenye amesema zaidi ya wananchi 11,000 wanatarajiwa kulipwa fidia Januari 2023, ili kupisha ujenzi wa daraja la juu la kisasa la Jangwani na uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi Mkoani Dar es Salaam.
Kanyenye amesema, Wananchi watakaonufaika ni wenye nyumba, wamiliki wa ardhi na wapangaji ambapo katika eneo hilo la Bonde la Mto Msimbazi kutajengwa ‘City Park’ na daraja la juu la kisasa na idadi ya nyumba zitakazolipwa fidia ni 3,291 na wapangaji wenye mikataba.
Amesema, “Taratibu za kulipa fidia kwa watu zaidi ya 11,000 na nyumba 3,291, wamiliki wa ardhi na wapangaji wenye mikataba zimekamilika na matarajio Januari, mwakani hatua hiyo itaanzwa kwa kuzingatia sheria.”
Aidha, ameongeza kuwa tathmini inaendelea na kwamba gharama za malipo ya fidia zitatolewa baada ya taratibu kukamilika huku akibainisha kuwa, “Serikali imepanga kurudisha uoto wa asili katika eneo hilo, kwa kujenga ‘City park’ kubwa ya kisasa kama Ulaya ambapo hekta zilizopo 420 kwa eneo lote, zinatosha kufanya kuwa sehemu ya tofauti yenye vivutio vingi.”