Wamiliki wa simu za Huawei zinazozalishwa na Kampuni kubwa ya China watakumbwa na pigo la aina yake la kutotumia YouTube na Google Map.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Kampuni ya Google ya nchini Marekani kutekeleza agizo la Rais Donald Trump lililopiga marufuku makampuni ya Marekani kuyauzia teknolojia makampuni ya China.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa kampuni ya Huawei kwani hawataweza kutumia tena program maarufu ya simu za Android ya ‘OS’ pamoja na huduma nyingine.
Kwa mujibu wa ripoti ya StatCounter, Android OS ilichukua zaidi ya 75% ya soko la hisa hadi Aprili 2019, ikifuatiwa na iOS ya iPhone yenye 23%.
Idara ya Biashara ya Marekani iliingiza kampuni ya Huawei kwenye orodha ya makampuni yaliyodaiwa kutishia usalama wa taifa hilo kwa kutoa huduma ya teknlojia kwa Iran. Makampuni ya Marekani yatahitaji leseni maalum ya Serikali kufanya biashara yoyote na Huawei.
Hata hivyo, Makamu wa Rais wa kampuni hiyo ambayo mwaka jana tu iliuza simu zaidi ya Milioni 200, Tim Watkins amewaambia waandishi wa habari kuwa walijiandaa tangu mwaka jana walipona dalili za mgogoro mkubwa wa kiuchumi kati ya China na Marekani, na sasa wanakamilisha mfumo wao mpya usiotegemea teknolojia ya Marekani.
Hivyo, aliwataka watumiaji wa simu hizo kuwa wavumilivu wakati wanakamilisha mfumo huo.