Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema inajitahidi kuboresha mazingira wezeshi kwa watu wenyeulemavu kwenye sekta zote za kijamii zikiwemo Usafiri wa umma, Elimu na Afya kwa kuzingatia na kurahisisha mahitaji yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo hii leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati akizungumza na ujumbe kutoka Shirika la kimataifa la Christian Blind Mission – CBM, waliofika kumtembelea.
Amesema, Serikali ikiwa kwenye mchakato wa kutoa huduma za Bima ya afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba, kipaumbele zaidi kimezingatiwa kwa watu wenyeulemavu, Zanzibar huku akieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Shirika hilo kupitia Wizara ya Afya Zanzibar.
Akizungumzia sera ya watu wenyeulemavu ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali inatekeleza sera hiyo kwa vitendo kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya jamii hiyo, na majengo yote ya umma inaweka mkazo zaidi kwa mahitaji yao ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo na ofisi za Serikali kufikiwa na watu wajamii zote ikiwemo huduma za ngazi na vyoo kuwa na mazingira rafiki kwa watu wote.