Serikali nchini, imetakiwa kuweka mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu wa uziwikutoona na kuwapa kipaumbele katika huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo haki zao za msingi za kibinaadamu.
Rai hiyo imetolewa na mmoja wa watu wenye ulemavu wa uziwikutoona, Mwanaasha Abdalah ambaye ameesema jamii imekuwa ikiwaweka kando katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kukwamisha ushiriki wao katika ujenzi wa nchi
Amesema, “Kwa miaka mingi kundi la watu wenye uziwikutoona limekuwa likisahaulika hasa kwenye fursa za maendeleo, pia kumekuwa na uelewa mdogo kwa baadhi ya wafanyakazi wa Serikali katika sekta mbalimbali, wadau na jamii kuhusu uwepo wa watu ambao ni viziwiwasioona, uwezo wetu, mahitaji yetu, na changamoto tunazopitia.”
Bi. Mwanaasha ameongeza kuwa, Serikali imepiga hatua ya kuwatambua kama kundi linalojitegemea la watu wenye ulemavu wa uziwikutoona kwa kutengeneza sera, sheria na mikakati mbalimbali kama vile mkakati wa taifa wa elimu jumuishi, kuanzishwa kwa dawati maalum TAMISEMI kwa ajili ya watu wenye uziwikutoona.
Ameitaja hatua nyingine kuwa ni kuanzisha vituo 10 katika shule za msingi kwa ajili ya wanafunzi wenye uziwikutoona, huku akidai utekelezaji wake bado unasuasua, akitolea mfano mazingira ya upatikanaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na ulinzi siyo rafiki kwa viziwiwasiyoona.
Aidha ameongeza kuwa, kutokuwepo kwa ujuzi au uelewa baina ya watumishi wa nafasi mbalimbali za serikali juu ya namna ya kuwasiliana nao kwa kuzingatia umuhimu wa kundi hilo, na kuishauri serikali kuangalia upya vigezo vya mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na Halmashauri haswa sharti la kuwa na kikundi cha kuanzia watu watano ambao wanatoka eneo moja.
”Tunafahamu kuwa tarehe 26/2/2021 Serikali ilitoa Mwongozo mpya wa kuwapatia watu wenye ulemavu mikopo wakiwa katika kikundi cha watu wawili au mmoja badala ya watano, lakini Mwongozo huo hautekelezwi, tunaiomba Serikali iweze kutekeleza Mwongozo huo ili na sisi tuweze kunufaika na mikopo hiyo ya halmashauri,” amesema Mwanaisha.
Taasisi ya Sense International Tanzania kupitia mradi wa WEZESHA VIJANA imewapatia mafunzo ya ujasiriamali na mitaji kwa vijana 33 nchini Tanzania wenye uziwikutoona ili waweze kujitegemea kwa msaada wa ushauri kutoka kwa maafisa biashara wa Wilaya na shirika la Youth With Disabilities Organazation (YoWDO).