Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewaagiza Wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya wilaya kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika hukumu.

Ametoa maagizo hayo maagizo jijini Dodoma alipozungumza na Wenyeviti pamoja na Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa nchi nzima kupitia Video (Video conference).

‘’Nasisitiza wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya mtumie lugha ya Kiswahili wakati wa kuandika hukumu zenu kama alivyoagiza  Rais Dkt. John Pombe Magufuli.’’ alisema Lukuvi.

Aidha, Lukuvi amewataka pia wenyeviti hao wa Mabaraza kuchapa hukumu za maamuzi wanayotoa wao wenyewe bila kutegemea Makarani na hukumu hizo zitoke kwa wakati na kusisitiza kuwa katika dunia ya leo suala la uzembe halina nafasi.

Aidha ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo uchache wa watumishi kwenye baadhi ya ofisi za Mabaraza ya Ardhi lakini watendaji hao wanatakiwa kuwajibika na kuacha visingizio pamoja na kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa serikali iko katika juhudi za kuhakikisha inajaza nafasi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa ni wajibu wa watendaji wa mabaraza ya ardhi kufanya kilicho sahihi na kuwa wabunifu sambamba  na kuwajibika kwa kutoa hukumu kwa wakati  na kusisitiza wananchi masikini wanategemea sana matumizi ya Kiswahili.

‘’Maamuzi yetu kama wenyeviti wa Mabaraza yawe rahisi na sisi tuwe wa kwanza kuwasaidia wananchi na kila mwenyekiti atekeleze maamuzi haya kwa lugha ya Kiswahili’’ alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi amesema, wapo wananchi waliokosa haki zao ama kuchelewa kukata rufaa kutokana na kutokujua kilichoandikwa katika hukumu kwa kuwa kimeandikwa kwa kiingereza.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 8, 2021
Video: Mawaziri, wasanii jukwaa moja