Beki na nahodha wa mabingwa wa soka nchini England Leicester City Wes Morgan amesema hawaihofii klabu yoyote katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Morgan amesema maneno hayo zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA halijapanga ratiba ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa.
Beki huyo aliyefunga moja ya mabao mawili yaliyowapeleka kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Sevilla CF, amesema wamefika kwenye hatua hiyo kutokana na kikosi chao kuwa bora, hivyo hawana shaka wala hofu ambayo inaweza kuwaingia kwa kuigopa klabu nyingine yoyote.
“Tunataka kudhihirisha ubora watu, tupo tayari kupangwa na klabu yoyote kwenye hatua ya robo fainali, najua dunia inasubiri kuona tutapangwa na nani, lakini hilo halitupi hofu kabisa, tupo hapa kwa ajili ya kupambana na sio kuhofia.” Alisema Morgan.
Leicester City walifanikiwa kuingia kwenye hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa jumla ya mabao matatu kwa mawili dhidi ya Sevilla CF, na kujiunga na klabu nyingine kama Real Madrid, FC Bayern Munich, Juventus, FC Barcelona, Atletico Madrid, AS Monaco pamoja na Borussia Dortmund .