Wagonga Nyundo wa jijini London ‘West Ham United’ wanawasubiri wanasheria wa Arsenal kupitisha uhamisho wa Nahodha na Kiungo wao Declan Rice kwenda Emirates Stadium.
Arsenal wana matumaini ya kukamilisha usajili wa Rice kabla ya kusafiri kuelekea Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Uhamisho wa kiungo huyo utaigharimu Arsenal kiasi cha Pauni Milioni 105, ambayo itagawanywa kwa malipo ya awali ya Pauni Milioni 100 kisha baadae watalipa nyongeza ya Pauni Milioni 5.
Usajili wa nahodha huyo wa West Ham utavunja rekodi ya uhamisho ya Pauni Milioni 72 ambayo Arsenal walilipa kumsajili winga Nicolas Pepe kutoka Lille mwaka 2019.
Kiwango cha fedha ambacho Arsenal wametumia kumsajili Rice kinazidi kiasi cha Chelsea walichotumia kumsajili kiungo wao, Enzo Fernandez kutoka Benfica Janauri mwaka huu. Chelsea walilipa Pauni Milioni 106 kumnyakua mshindi huyo wa Kombe la Dunia.
Arsenal pia inatarajia kuthibitisha usajili wa beki, Jurrien Timber kutoka Ajax huku wakitazamiwa kumtumia kwenye mchezo wao wa kirafiki dhidi ya FC Nurnbeg, kesho Alhamisi (Julai 13).
Timber amekamilisha vipimo vya afya ambapo klabu ya Arsenal ilitumia Pauni Milioni 38 kumsajili mlinzi huyo kwa mkataba mrefu.
Arsenal italipa Pauni Milioni 34 huku kiasi kitakachobaki kitalipwa kutokana na kiwango kitakachooneshwa na mlinzi huyo.