Wagonga Nyundo Wa Jijini London (West Ham Utd) wapo tayari kumsajili kiungo wa Man Utd, Michael Carrick ambaye kwa sasa anakabiliwa na mazingira magumu huko Old Trafford.

Man utd wamekua kimya juu ya mustakabali wa Carrick, kutokana na mkataba wake aliousaini msimu uliopita kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Meneja wa West Ham Utd, Slaven Bilic, amesisitiza kuwa tayari kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, kama mbadala wa kiungo kutoka nchini Cameroon, Alex Song.

Song anatarajia kuondoka mwishoni mwa msimu huu, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo na kwa sasa hayupo kwenye mikakati ya meneja huyo kutoka nchini Croatia.

Hata hivyo Bilic, amesema yu radhi kumsajili Carrick endapo atakubali masharti ya klabu ya West Ham Utd ya kusainishwa mkataba wa mwaka mmoja, kutokana na kigezo cha umri wake kuvuka miaka 30.

Carrick, anaonekana kuwa na uzoefu mkubwa katika ligi ya nchini England tofauti na ilivyo kwa kiungo mwenye umri wa miaka 17 Havard Nordtveit, ambaye yupo kwenye mipango usajili wa Bilic.

Kiungo huyo kutoka nchini Norway ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Borussia Mönchengladbach ya nchini Ujerumani, anapewa nafasi kubwa ya kusajiliwa mwishoni mwa msimu huu.

Michael Carrick alianza kucheza soka nchini England akiwa na klabu ya West Ham Utd kuanzia mwaka 1999–2004, baada ya kukuzwa katika kituo cha kuendeleza na kukuza vipaji kwa vijana cha klabu hiyo.

Baada ya hapo alisajiliwa na Spurs ambapo alidumu huko kwa miaka miwili kabla ya kusajiliwa na Man Utd chini ya utawala wa Sir Alex Ferguson mwaka 2006

Kwa hiyo kama atasajiliwa na West Ham Utd mwishoni mwa msimu huu, Carrick atakua anarejea nyumbani na pengine huenda akamalizia soka lake kwenye klabu hiyo yenye maskani yake magharibi mwa jijini London.

Mayweather apinga ushindi wa Pacquiao kwa Brandley, amtaka Brandley afanye hili
Waingereza Wamkebehi Neymar, Wamshindanisha Na Njonjo