Kiongozi wa chama cha Ford cha Kenya, Moses Wetangula amechaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la Kitaifa la Kenya akichukua nafasi ya Justin Muturi anayemaliza muda wake.
Wetangula, ambaye ni mwanasiasa wa Kenya Kwanza alimshinda mpinzani wake katika kingang’anyiro hicho, Kenneth Marende wa chama cha muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, kinachoongozwa na Raila Odinga.
Wetangula, ameshinda kiti hicho baada ya kupata kura 215 dhidi ya kura 130 za Marende wakati wa awamu ya kwanza ya upigaji kura uliofanyka nchini humo.
Upigaji kura ulipangwa kufanyika kwa awamu ya pili, kwa kuwa hakuna mgombea yeyote aliyepata theluthi mbili ya kura zilizohitajika, lakini Marende alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho hivyo kumuacha Wetangula kuwa mshindi.
Tukio la kujiondoa kwa mpinzani wake, kulimfanya Wetangula kuapishwa mara moja baada ya kula kiapo cha ofisi katika ukumbi wa Bunge, huku Spika anayeondoka Muturi akimpongeza rasmi na kumkabidhi wadhifa huo.
Upigaji kura huo ulikuja baada ya taharuki katika hatua za awali za kikao cha Bunge la Kitaifa ambapo baadhi ya wabunge wanaoungwa mkono na Azimio walipinga kugombea kwa Wetangula wakisema hastahili kuwania kiti cha Spika.
Wetangula alikuwa amechaguliwa kuhudumu kwa muhula mwingine akiwa Seneta wa Bungoma kwenye uchaguzi wa Agosti 8, 2022, lakini akajiuzulu wadhifa huo ili kuwania Uspika wa Bunge la Kitaifa.