Watu wasiojulikana wanaosadikika kuwa ni wezi, wamevamia Kanisa la Makutano PAG lililopo Lurambi nchini Kenya na kuiba mali ambayo thamani yake haijajulikana.

Kiongozi wa wanawake wa kanisa hilo, Mama Prisca Orembo amesema kuwa walipata taarifa kuwa tukio hilo limetokea Jumapili, Aprili 18, 2021 majira ya asubuhi.

“Tumepata taarifa kuwa kulikuwa na tukio la wizi kanisani kwetu. Tulipofika pale, tulithibitisha kuwa wezi walivamia na kuvunja milango ya kanisa na kwenye nyumba ya Mchungaji,” Mama Prisca aliiambia Citizen Digital.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyokuwa katika eneo la tukio, wezi hao waliiba nguo za ndani za Mchungaji na vyakula vilivyokuwa jikoni.

“Wezi hata wanaiba manguo za ndani za pastor wanaenda kuuza, hii ni nini?” mfanyakazi mmoja wa kanisa ambaye pia ni muumini wa kanisa hilo alikaririwa na Citizen TV.

Naye Wycliffe Sajida, mchungaji wa kanisa hilo ambaye anaishi nyumba ya jirani na kanisa hilo alisema naye pia alipoteza kila kitu.

“Kwangu pia walivamia, waliiba kila kitu, walichukua suti mbili, fulana tano, sare mbili za viatu, jiko la gesi na Sh. 2,500 za Kenya,” alisema Mchungaji Wycliffe.

Jeshi la Polisi limethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na linazifanyia kazi kuhakikisha waliohusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Rais Samia akemea uzandiki
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 17, 2021