Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani – WFP, Martin Frick amesema mapigano yanayoendelea nchini Sudan yanaweza kuzitumbukiza nchi Afrika Mashariki katika mgogoro wa kibinadamu.
Flick ameyasema hayo mapema hii leo na kuongeza kuwa theluthi moja ya wakazi wa Sudan walikumbwa na baa la njaa kabla ya mapigano kuanza Aprili 15, 2023 na sasa wanakabiliwa na mfumuko wa bei, uhaba wa bidhaa muhimu pamoja na chakula.
Amesema, nchi jirani za Chad na Sudan Kusini ambazo zimewapokea maelfu ya wakimbizi tangu mapigano yalipoanza wiki mbili zilizopita, zinakabiliwa na ongezeko kubwa la kupanda kwa bei za bidhaa, na kwamba bei za vyakula zimepanda kwa asilimia 28 katika kipindi cha muda mfupi.
Hatua hiyo, imesababishwa na Kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan kupambana na Naibu wake, Mohammed Hamdan Dagalo ambaye ni kiongozi wa kundi la wanamgambo wenye ushawishi mkubwa na wanaofahamika kama Vikosi vya Msaada wa Haraka – RSF.