Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), limesema linaamini kwamba janga la virusi vya corona halina uwezekano wa kumalizika katika miezi ya karibuni na wala halina dalili ya kumalizika mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mpango wa dharula wa shughuli za kiafya WHO, Michael Ryan, amesema anadhani ni mapema kufikiria kwamba watalimaliza janga hili kufikia mwishoni mwa mwaka.
Amesema kinachoweza kumalizwa ikiwa ulimwengu utakuwa makini ni idadi ya watu kulazwa hospitali kutokana na virusi hivyo au vifo na matatizo mengine yanayosababshwa na janga hilo.
Nchi mbalimbali zinapambana kuhakikisha raia wake wanapata chanjo ya Covid-19 wakati janga la virusi vya Corona likiendelea.
Aidha, WHO imetoa wito kwa nchi mbalimbali kujiepusha kuondoa haraka shughuli za kudhibiti virusi vya corona, kutokana na kuwepo chanjo.