Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Joe Phaahla amesema kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ndani ya siku tano zilizopita kutokana kugundulika kwa aina mpya ya kirusi cha corona kinachopelekea kuongezeka kwa maambukizi nchini humo
Wanasayansi nchini humo wanajaribu kutathmini ni asilimia ngapi ya visa vipya ambavyo vimesababishwa na aina mpya ya kirusi huku wakiingiwa na wasiwasi wa aina hiyo mpya ya kirusi kinachotajwa kujibadili kwa kasi kubwa na kuenea kwa kwa haraka miongoni mwa vijana.
Aidha Kirusi hicho aina ya B.1.1.529, pia kimeripotiwa nchini Botswana na Hong Kong miongoni mwa wasafiri waliotoka Afrika Kusini.
Wataalamu wa shirika la afya duniani WHO watakutana leo kutathmini kirusi hicho na ikiwa watakipatia jina la kigiriki.
Wakati huohuo serikali ya Uingereza imetangaza kuzifuta safari za ndege kutoka Afrika Kusini na nchi nyingine tano za Kusini mwa afrika kuanzia Novemba 26, 2021 yeyote atakayeingia kutokea katika nchi hizo atapaswa kufanya vipimo vya corona.
Waziri wa afya wa Uingereza Sajid Javid amesema kuna wasiwasi aina hiyo mpya “inaweza kuambukiza zaidi” kuliko aina kuu ya kirusi cha delta, na kwamba chanjo zilizoko kwa sasa zinaweza kuwa na ufanisi mdogo dhidi yake.
Afrika Kusini imerekodi zaidi ya visa vipya 200 kwa siku wiki iliyopita na kufikia Jumatano ya Novemba 25 maambukizi ya kila siku yaliongezeka na kufikia 1,200. Afrika Kusini imechanja asilimia 41 ya watu wazima na inazo dozi milioni 16.5 za chanjo ya corona.
Afika Kusini yenye idadi ya watu milioni 60, limerekodi zaidi ya visa milioni 2.9 vya COVID-19 na vifo ni zaidi ya 89,000.