Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema kuwa takribani watu milioni 44 wanaweza kuambukizwa virusi vipya vya corona (covid-19) barani Afrika, na watu 190,000 wanaweza kupoteza maisha, kama hatua za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo zitashindwa.
Taarifa hii ya WHO imekuja wakati ambapo Afrika imeripoti jumla ya visa 53,200,000 na vifo 2,027.
WHO wameeleza kuwa kati ya watu milioni 3.6 na milioni 5.5 wanaweza kulazwa hospitalini kutokana na virusi hivyo, na watu kati ya 82,000 na 167,000 wanaweza kuwa katika hali ya mahututi.
Hata hivyo, takwimu hizi zinaonesha kiwango cha chini kwa kulinganisha na taarifa za awali za WHO, ambapo walisema inakadiriwa kuwa covid-19 ingekuwa chanzo cha vifo vya watu 300,000 barani Afrika hadi sasa na kusababisha umasikini wa kutupwa kwa watu takribani milioni 29.
Imeeleza kuwa kushuka kwa kiwango kilichokadiriwa awali kunatokana na mazingira ya Afrika, ikiwa ni pamoja na kuwa na vijana wengi zaidi ya wazee.
Aidha, imeeleza kuwa huenda katika miaka ya hivi karibuni kukawa na mlipuko zaidi ya virusi hivyo, na nchi zinazoweza kuathirika zaidi ni pamoja na Algeria, Afrika Kusini na Cameroon.
“Covid-19 inaweza kuwa sehemu ya maisha yetu kwa miaka mingi kama Serikali husika hazitachukua hatua stahiki. Kiasi cha mlipuko ni kikubwa na aghali zaidi kuliko hatua zinazochukuliwa na baadhi ya Serikali,” taarifa ya WHO imeeleza.