Mshambuliajin wa klabu ya Crystal Palace inayoshiriki Ligi Kuu ya England Wilfred Zaha, amesema anapata wakati mgumu kufungua kurasa za mitandao ya kijamii anazozimiliki, kwa kuhofia maneno ya kibaguzi ambayo hutumwa na watu wanaoendekeza dhambi hiyo.
Mapema mwezi huu kijana wa miaka 12, alishtakiwa kwa kuandika maneno ya kibaguzi kwa mshambuliaji huyo wa Crystal Palace katika mtandao wake wa Instagram (Direct Message).
Zaha anasema ilimbidi pia kujiondoa katika mtandao wa twitter katika simu yake kutokana na kauli za kibaguzi kuzidi kila kukicha.
“Kwa mchezaji mweusi, kwa mfano kuwa katika mtandao wa Instagram sio kitu cha furaha tena.” Zaha aliiambia CNN.
“Haufurahii wasifu wako kwa sababu unaogopa hata kuangalia ujumbe unaotumwa moja kwa moja tena. Unaweza kukutana na kitu chochote.
“Sina mtandao wa Twitter katika simu yangu kwa sababu mara zote utaenda kukutana na jumbe za kibaguzi, hasa baada ya mchezo.
“Kijana huyo wa miaka 12 aliwasiliana na wachezaji wengine watatu, na kuwatumia maneno ya kibaguzi pia, hii sio SAWA.”
Instagram inayomilikiwa na Facebook, imekuwa ikishutumiwa kwa kutokulinda haki za wachezaji weusi, kutokana na ubaguzi wanaupata kutoka katika mtandao huo.
Wiki iliyopita, Facebook na Instagram walitangaza watatengeneza timu itakayo pambana na ubaguzi katika mitandao yao.
“Ubaguzi hautavumiliwa katika Facebook na Instagram.” msemaji wa Facebook aliiambia CNN.