Wagonga nyundo wa jijini London (West Ham United) wanakaribia kumsajili kiungo kutoka nchini Ureno na klabu ya Sporting Lisbon William Carvalho.
Taarifa zilizotangazwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports cha England, zimeeleza kuwa West Ham Utd, wapo katika hatua za mwisho za makubalino ya usajili wa kiungo huyo, na kuna uwezekano wa dili hilo kukamilishwa ndani ya juma hili.
The Hammers wamekua na mazungumzo na uongozi wa Sporting Lisbon kwa kipindi cha majuma mawili, na waliwahi kutuma ofa mara mbili zilizomlenga kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 lakini zilikataliwa.
Kituo hicho cha televisheni kimeongeza kuwa, West Ham Utd wamejizatiti kutoa kiasi cha Pauni milioni 40 ili kukamilisha dili la Carvalho, ambaye anaaminiwa huenda akafanikisha harakati za kuisuka vyema safu ya kiungo ya wagonga yundo hao.
Carvalho hakujumuishwa kwenye kikosi cha Sporting Lisbon kilichocheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa ligi ya mabingwa barani Ulaya katikati ya juma lililopita dhidi ya Steaua Bucharest, uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Hatua hiyo inaaminiwa huenda ilikua ni sehemu ya kukubaliwa kwa dili la West Ham Utd, huku Sporting Lisbon wakihofia kufanya maamuzi ya kumchezesha mchezaji huyo kutokana na kanuni za michuano ya Ulaya ambazo zingeonyesha wamemsajili kwenye michuano hiyo.