Kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Willian Borges da Silva, amemchana hadharani aliyekua meneja wa kikosi cha Chelsea Antonio Conte, kwa kusema engeendelea kubaki klabuni hapo, ingekua sababu tosha ya kuachana na The Blues msimu huu, na kuelekea mahala pengine.
Willian ambaye alikua anahusishwa taarifa za kutaka kusajiliwa na Man Utd kwa England pamoja na FC Barcelona ya Hispania, amesema Conte alikua kikwazo kikubwa katika maamuzi yake ya kuendelea kusalia klabuni hapo, kutokana na tabia zake za kushindwa kumtumia ipasavyo.
Amesema wakati mwingine meneja huyo kutoka nchini Italia, alikua akimfanyia kusudi kutomuanzisha katika kikosi cha kwanza, na hatua hiyo ilimchosha na kuona alikua hana nafasi tena ya kucheza kama ilivyokua zamani.
“Angeendelea kubakia hapa ningeondoka na kwenda kucheza soka mahala pengine,” Willian alimjibu mwandishi wa gazeti la Evening Standard:
“Nipo hapa kwa ajili ya kucheza, na kama ninapata nafasi ya kucheza mara kwa mara, kwa nini nifikirie kuondoka?” Alihoji kuingo huyo.
“Ilifikia hatua nikaamini sina nafasi tena ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Chelsea, na nilijipanga kuihama klabu hii, kutokana na kuchoshwa na mipango ya kocha yule.”
“Kwa sasa nimeanza kuona thamani yangu kikosini, ninaamini nitakua miongoni mwa wachezaji watakaopewa nafasi mara kwa mara, chini ya meneja mpya,”
“Najua ni mapema mno kusema maneno haya, lakini ushirikiano mzuri ninaoupata kutoka kwa meneja Sari, unanionyesha matarajio yangu na kwa upande wake katika kunitumia mara kwa mara, ili niweze kuwa miongoni mwa wachezaji watakaofanikisha malengo yaliyokusudiwa msimu huu.”
Meneja Maurizio Sarri alikabidhiwa kikosi mwezi Julai, na tayari ameanza vizuri mshike mshike wa ligi kuu ya England, kwa kupata ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Huddersfield Town mwishoni mwa juma lililopita.