Kiungo Jack Wilshere na mshambualiji Alexis Sanchez wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kitakachoanza katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi wa michuano ya Europa League dhidi ya FC Cologne siku ya Alkhamis.
Wilshere hajawahi kucheza katika kikosi cha Arsenal tangu mwanzoni mwa msimu huu, na ilidhamniwa huenda angeondoka kutoakana na changamoto ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25, alirejea klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita akiwa majeruhi, baada ya kumaliza mkataba wa mkopo wa kuitumikia AFC Bournemouth.
Kwa mara ya mwisho aliitumikia Arsenal katika mchezo dhidi ya Watford miezi 13 iliyopita.
Kwa upande wa Sanchez ambaye alishindwa kufanikisha uhamisho wake wa kuelekea Man city siku ya mwisho ya dirisha la usajili majira ya kiangazi, alicheza mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya AFC Bournemouth akitokea benchi.
Katika hatua nyingine washambuliaji Theo Walcott, Olivier Giroud na beki wa pembeni Mathieu Debuchy huenda wakapata nafasi ya kuanza katika mchezo huo wa Europa League dhidi ya FC Cologne, ambao wanashika mkia katika msimamo wa ligi ya nchini Ujerumani.