Takribani watu 12 wameuawa kutokana na mapigano kati ya wanamgambo wanaounga mkono serikali pinzani na kuharibu hospitali 6 katika mji mkuu wa Libya Tripoli, hatua iliyozua hofu ya kuzuka kwa mvutano wa kisiasa unaoweza kusababisha mgogoro mkubwa.
Milio ya silaha na milipuko vilisikika katika wilaya kadhaa za mji huo usiku wa kuamkia leo na moshi ulionekana ukifuka kutoka katika majengo yalioharibiwa vibaya.
Wizara ya afya mjini Tripoli katika taarifa yake ya awali imesema kwamba watu 12 wameuwawa katika ghasia hizo na wengine 87 wamejeruhiwa.
Hospitali sita zilishambuliwa na magari ya kubeba wagonjwa hayakuweza kufika katika maeneo ambayo yameathiriwa na mapigano.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na waziri mkuu Abdulhamid Dbeibah imesema mapigano yamezuka baada ya kushindwa kwa mazungumzo ya kuepusha umwagaji damu katika mji huo.