Kiswahili kinaendelea kuwa ‘dhahabu’ inayong’arisha matukio na vitu vingi duniani, na sasa kitasikika kwenye wimbo wa Beyonce Knowles uliovuta usikivu wa watu wengi duniani utakaotumika kwenye filamu inayosubiriwa kwa hamu ya ‘The Lion King’.

Mwanzoni, katika wimbo huo uliopewa jina la ‘Spirit’, inasikika sauti ya mtu akiimba kwa kupaza sauti akitoa heshima kwa Mfalme, “uishi kwa muda mrefu Mfalme.” Wimbo huo ni moja kati ya vitu vinavyoiinua filamu hiyo hata kabla yaijatoka rasmi, kutokana na ushawishi mkubwa wa Malkia Bey kwenye kiwanda cha burudani duniani kote.

Sauti hiyo inasikika mara mbili kabla ya Beyonce kuingia na kushusha mashairi yanayotoa ujumbe unaoendana na filamu ya ‘Lion King’, ambayo inamuelezea mtoto Simba anayepambana kuwa kama baba yake. Malkia Bey yeye ameimba Kiingereza.

Filamu hiyo iliyoongozwa na Jon Favreau inatarajiwa kutoka rasmi Julai 17, 2019 lakini tayari imeshazinduliwa nchini Marekani na kupewa mapokezi ya aina yake.

Katika uzinduzi uliofanyika wiki hii, Beyonce na familia yake walikuwa miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria.

‘The Lion King’ imeandaliwa na Destiny na waalikwa walioonjeshwa ladha siku ya uzinduzi, wameitaja kuwa moja kati ya filamu bora zaidi zilizowahi kutoka.

“The Lion King ni filamu kubwa, sijawahi kuona kitu kama hiki. Naamini kitabadili jinsi tulivyokuwa tunatazama filamu daima,” alitweet Adam B. Vary wa Buzzfeed.

Filamu hii imebeba maudhui ya Kiafrika yenye mtazamo wa maisha ya Kifalme na harakati zinazofanana na maisha hayo.

Simba anafuata nyayo za maisha ya baba yake aliyekuwa Mfalme, ‘Mfalme Mufasa’. Lakini tangu aanze kukanyaga nyayo hizo anakutana na harakati za mapambano dhidi yake na changamoto nyingine.

Kama ilivyokuwa ‘Black Panther’, ‘Lion King’ itakuwa kubwa inayohusu Afrika na lugha yetu adhimu ya Kiswahili itakuwa ikipepea.

Majina ya wahusika kwenye filamu hiyo pia yamepewa uhalisia wa majina yanayopatikana Afrika.

Usikilize hapa:

RC Makonda aanza maandalizi ya mkutano wa SADC
NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha sita