Siku chache baada ya Mataifa ya Afrika ya Magharibi, kudai kuwa yangetuma kikosi cha kumrejesha madarakani kiongozi wa nchi ya Niger aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum tayari ukanda huo umesitisha mkutano muhimu wa kijeshi ulikuwa ukilenga kutatua mzozo wa Taifa hilo.
Awali, Wakuu wa Majeshi ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi – ECOWAS, walikuwa wakutane siku ya Jumamosi (Agosti 12) katika mji mkuu wa Ghana, Accra, lakini jioni ya Ijumaa kulitolewa tamko la kuuakhirisha mkutano huo kwa muda usiojulikana.
Mkutano huo, ulikuwa umeandaliwa ili kuwaeleza viongozi wa ECOWAS juu ya njia bora zaidi za kuunda na kutuma kikosi hicho cha dharura nchini Niger, na bado ECOWAS bado haijafafanuwa undani wa kikosi hicho wala ratiba ya hatua zake, huku wakisisitiza kutaka suluhisho la amani.
Hata hivyo, kuahirishwa kwa mkutano huo kulitangazwa wakati maelfu ya wananchi wa Niger wakikusanyika kuunga mkono jeshi lao mbele ya kituo kimoja cha jeshi la Ufaransa chenye Wanajeshi zaidi ya 1,500 wanaoshiriki vita dhidi ya makundi ya kigaidi Ukanda wa Sahel.