Waendesha Baiskeli wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya Barabara na lugha ya ishara, pindi wanapokuwa Barabarani kwa lengo la kuwasiliana wao kwa wao na watumiaji wengine wa barabara wakiwemo waenda kwa miguu na Madereva wa magari.
Elimu hiyo, imetolewa Septemba 18, 2023 Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma na na Askari G.4664 Koplo Emmanuel ambaye amewataka wapanda Baiskeli hao kunyoosha mkono wa kulia au kushoto pindi wanapotaka kukata kona kwenda kuingia barabara nyingine.
Aidha, wapanda baiskeli hao pia wametakiwa kushuka na kukokota baiskeli wakati wa kuvuka upande wa pili wa barabara, kupakia abiria mmoja, kuvaa nguo zenye kuakisi mwanga hasa nyakati za usiku na kufanya matengenezo ya vyombo vyao ikiwemo ufungaji wa taa za mbele na breki.
Elimu hiyo, imelenga kuondoa ajali za barabarani kwa watumiaji hao wa barabara na kuwasaidia kuepuka mgongano wa ni wapi wanaelekea pindi watakapotaka kubadilisha njia kwa pande zote wawapo safarini.