Wizara ya Afya, imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa elimu juu ya tahadhari ya kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza, kufuatia Mamlaka ya Hali ya hewa kutangaza uwepo wa mvua kubwa za mafuriko, Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Shinyanga, Flora Sagasaga amesema elimu hiyo ina faida kubwa kwa Wananchi.
Sagasaga ambaye pia ni Diwani wa kata ya Mwalugulu amebainisha hayo wakati akizungumza na Elimu ya Afya kwa Umma, juu ya mikakati waliyoiweka kuhakikisha elimu inafika kila kitongoji katika Halmashauri hiyo.
Amesema, “tumeshasikia taarifa kuwa kutakuwa na mvua kubwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo mkoa wetu wa Shinyanga na sisi kama viongozi tumeshaanza kuchukua tahadhari, mimi katika kata yangu kati ya vijiji 6, vijiji 2 El nino ikiingia patakuwa na hatari vijiji hivyo ni Igudu na Mwankima watu wanaishi mabondeni sana hulima mpunga, tumeshaanza kuwaambia watoke mabondeni ili kuondoa madhara.”
Aidha, Sagasaga ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa kuwa mstari wa mbele katika suala la uelimishaji katika kujikinga dhidi ya madhara ya mafuriko ikiwemo magonjwa ya mlipuko pamoja na msisitizo kwa kamati za maafa kuimarishwa huku baadhi ya Wananchi akiwemo Firiki Charles, Khadija Shaban Ng’hagala pamoja na pamoja Shija Lukenanga wamezungumzia umuhimu wa tahadhari ya mafuriko.
Kwa nyakati tofauti wamesema, “kama matangazo ambayo nimekuwa nikiyasikia kupitia vyombo vya Habari nasisitiza tu wazazi wenzangu tusiruhusu watoto kucheza karibu na kingo za maji, na vyombo vinavyosafiri visivuke maporomoko ya maji kwani si vyema kudharau nguvu ya maji”amesema Firiki Charles.
Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania – TMA, imeshatangaza uwepo wa mvua kubwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Shinyanga, Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Mara, Kigoma, Morogoro, Pwani, Dar Es Salaam, Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro ambapo Wizara ya Afya kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma imekuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii kuchukua tahadhari juu ya madhara yanayoweza kujitokeza.