Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amesema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2022, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 90.9 ambacho ni sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 121.
Waziri Mabula ameyasema hayo hii leo Februari 7, 2023 Jijini Dodoma na kuongeza kuwa makusanyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yameongezeka kwa Shilingi bilioni 33.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka wa Fedha 2021/22.
Amesema, “wananchi 6,211 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo, ikiwa ni sawa na shilingi 11,931,537,409.80 na Serikali inaamini kuwa fedha hizo zilizosamehewa zimeenda kuleta nafuu kwa wahusika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.”
Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassani alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi ambapo wananchi walio na malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia Julai hadi Desemba, 2022.