Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, kwa kushirikiana na Wizara ya fedha na Mipango inajipanga kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa jamii hasa makundi maalum.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima, amesema ushahidi unaonesha kuwa, yapo Makundi mengi ndani ya Jamii ambayo yanatamani kuchangamkia fursa za kiuchumi lakini wanashindwa kutokana na kutokuwa na taarifa ya wapi pakuanzia.
“Mwaka 2022 nilipata Bahati ya kutembelea Maonesho ya Saba Saba na kupita kwenye taasisi kadhaa za fedha ambapo nilibaini uwepo wa fursa ambazo wanajamii wengi hawazifahamu” amebainisha Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Kamishna wa sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamwaja amesema Jamii ina kila sababu ya kuelimishwa kuhusu fursa na matumizi ya fedha katika maisha yao ya kila siku na kubadili utaratibu wa nidhamu ya fedha kwa kuwa na utaratibu wa kuweka akiba.