Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ameongoza kikao cha kutoa maoni kuhusu Mpango Jumuishi na Endelevu wa kuratibu Wahudumu wa Afya Ngazj ya Jamii kilichowakutanisha Watumishi wa Wizara ya Afya na wadau.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, Prof. Nagu amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana umuhimu mkubwa katika utoaji wa huduma za afya hivyo kupitia kikao hicho cha kupitia Mpango huo itakuwa ni chachu katika uimarishaji wa huduma za afya ngazi ya jamii.
Amesema, “Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana umuhimu kwani wao ndio wanaosaidia kutoa elimu ya afya ngazi ya chini kabisa ya kijiji hivyo kupitia Mpango Jumuishi itakuwa chachu kubwa katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya jamii mfano elimu juu ya lishe, utapiamlo.”
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana mchango mkubwa katika kusambaza ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya afya hasa katika eneo la kinga dhidi ya magonjwa ngazi ya jamii, huku Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Prof. Pascal Ruggajo akisema kupitia Programu hiyo itasaidia kuondoa vikwazo katiika upatikanaji wa tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dkt.Tumaini Haonga amesema baadhi ya mikakati kabambe inayotumika katika uimarishaji wa huduma za afya ngazi ya jamii ni pamoja na kutoa elimu ya afya katika mapambano ya UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu na magonjwa ya mlipuko ya Kuhara na Kipindupindu.