Wizara ya Maliasili na Utalii Nchini, kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ya Sekta ya utalii, wanakusudia kuendelea kujiimarisha katika mikakati ya kupambana na matukio ya Ujangili.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wa matumizi ya mfumo wa kubadilishana taarifa wa EAC TWIX maafisa Intelijensia na Himasheria Jijini Arusha.
Dkt. Msofe ambaye alikuwa akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii amesema, Wizara hiyo itaendelea kutanua wigo wa Kimataifa, katika kupambana na kudhibiti vitendo vya ujangili.
Katika azma hiyo, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP, pia inatekeleza Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara – IWT, ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia – GEF na UNDP.