Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi kutotumia dawa bila maelekezo ya Daktari kwa madai ya kutibu virusi vipya vya corona, kwani hadi sasa hakuna dawa ya kutibu au kuzuia virusi hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi, Wizara hiyo imefafanua kuhusu matumizi ya baadhi ya dawa ambazo zimekuwa zikitajwa kutumika kwa madai kuwa zinatibu virusi vya corona.
“Wizara inapenda kuutaarifu umma kuwa mpaka sasa HAKUNA DAWA YA KUTIBU AU KUZUIA CORONA. Dawa zote zinatumika kwa kuzingatia mwongozo wa Daktari,” imeeleza taarifa hiyo.
“Dawa kama Azithromicyn hutumika kutibu magonjwa mbalimbali kama magonjwa ya mapafu itokanayo na bakteria na sio virusi. Dawa ya Aspirin hutumika kwa ajili ya maumivu, homa na magonjwa ya moyo kwa maelekezo maalum ya Daktari, Predinisiolone kwa magonjwa kama ya ngozi, pumu n.k na dawa za ARV kwa ajili ya wagonjwa wenye virusi vya UKIMWI,” imeongeza.
Mganga Mkuu ameeleza kuwa matumizi holela ya dawa hizo yanaweza kusababisha usugu wa dawa na kusababisha kutotibu tena magonjwa yanayotokana na bakteria. Pia, alieleza kuwa dawa kama Aspirin zina madhara makubwa zisipotumika ipasavyo kwani zinaweza kusababisha vidonda vya tumbo na kutokwa na damu.
“Kama dawa hizi zingekuwa zinatibu au kuzuia hili tatizo basi, vingelikuwa vimeshatumika sana huko Ulaya, Uchina na Marekani maana huko ndio zinazalishwa kwa wingi,” ameongeza.
Amewataka wananchi wanaohisi dalili za COVID-19 kutoa taarifa kwa kupiga namba 199 bila malipo.
Aidha, Profesa Makubi ameeleza kuhusu tiba asili ikiwa ni pamoja na hatua ya kujifukiza ambayo imeshika kasi mitandaoni.
Alisema kuwa Serikali inaelekeza kitengo cha Wizara ya Afya cha Tiba Asili/Tiba Mbadala na Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili kwa pamoja kutoa elimu kwa umma na ufafanuzi kuhusu Tiba Asili/Mbadala na njia za kujifukiza au kunywa.
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Serikali alisema kuwa hakuna sababu ya maiti za wapendwa wetu waliofariki kwa ugonjwa wowote ule kuzikwa nyakati za usiku au gizani.
Aliwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa familia zinashirikishwa kikamilifu katika kuandaa na kufanya mazishi kwa heshima zote za utu bila haraka na hofu.
JPM ashtukia ‘mchezo mchafu’ vipimo vya corona… papai, mbuzi wakutwa na corona
Viongozi wa Dini Morogoro waungana na serikali kupambana na Corona