Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya kuingia kwa ugonjwa wa Chikungunya nchini baada ya watu wanne waliotokea nchini Kenya kubainika kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu jijini katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam wakati akiongea na waandishi wa Habari.
“Mnamo tarehe 20, Mwezi Juni, 2018 wasafiri wanne wa familia moja waliotokea tena Mombasa nchini Kenya walishukiwa kuwa na ugonjwa huu baada ya kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa wa homa ya Chikungunya kwenye kutuo cha mpakani cha Holili kilichopo wilayani Rombo mkoani Kiliamanjaro”, alisema Ummy.
Waziri Ummy aliwatoa hofu wananchi kuwa Ugonjwa huu si mpya katika nchi yetu kwani hapa nchini uligundulika katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania, sehemu za Makonde katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji mnamo mwaka 1952 huku Jina la ugonjwa likiwa na asili ya Kimakonde lenye maana ya “kilichopinda” yaani hali ya kupinda mwili inayotokana na maumivu makali ya viungo kunakosababishwa na ugonjwa huu.
Kwa upande mwingine, Ummy alithibitisha juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini hususani katika jiji la Dar es salaam huku idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.
“Dengue ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani jijini Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Januari 2018. Hadi kufikia sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam. Vilevile ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani umewahi kuripotiwa katika miaka ya 2010, 2013 na 2014,” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameeleza dalili za ugonjwa wa Dengue zinashabihiana ambazo ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza siku ya 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya magonjwa haya. Wakati mwingine dalili za magonjwa haya yanaweza kufanana sana na dalili za 95ugonjwa wa malaria.