Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa maelekezo kwa wanafunzi 337 ambao matokeo ya mitihani yao ya kidato cha nne mwaka 2022 yamefutwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu kuomba kurudia tena Mitihani hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kati ya wanafunzi 337 ,wanafunzi 333 walifutiwa matokeo kutokana na udanganyifu huku wanafunzi 4 wakifutiwa matokeo kutokana na kuandika matusi katika mitihani yao.
Amesema, “Tungesema hawa wanafunzi warudie mitihani na wenzao wa kidato cha nne kwa utaratibu wa kawaida kama ilivyozoeleka ni kwamba serikali ingepata hasara zaidi ya Bilioni moja ila kwa utaratibu huu wa kuomba wenyewe kama Private Candidate na kufanya mtihani huo pamoja na wenzao wanaofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu kwa utaratibu utakaowekwa na NECTA basi itasaidia sana kupunguza gharama.”
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda
“Ni huruma tu imetumika hapa na kweli Baraza la Mitihani la Tanzania limetumia busara sana kwani watoto hawa wamejikuta tu wamebananishwa kwenye pembe ya udanganyifu penda wasipende na wengine kujikuta wanapewa adhabu na kujikuta wanabeba makosa ya taasisi yao ndio maana tumeamua kuwaruhusu hawa wanafunzi 337 kufanya maombi ya kurudia mitihani hii,” amesema Prof. Mkenda
Prof. Mkenda amebainisha kuwa utaratibu wa kurudia mitihani hiyo kwa wanafunzi hao utakwenda sambamba na mitihani ya kidato cha sita ambao unatarajiwa kuanza Mei 2,2023, hivyo watawekewa utaratibu wa kuchanganyika pamoja wakati wa kurudia mitihani hiyo.
Pia amewataka watanzania kwa ujumla kukemea kwa pamoja matukio ya wizi wa mitihani kwani inafundisha watoto udanganyifu na wizi ,pia inaondoa uweledi pamoja na kuwanyima haki watahiniwa ambao hawajashiriki katika wizi huo ila wamefaulu kwa jitihada zao wenyewe.
“Kufuta matokeo ya mtihani kwa Wanafunzi wetu ni uchungu mkubwa kwani kuna baadhi ya wanafunzi watashindwa kurudia mitihani katika duru zinazofuata kutokana na changamoto mbalimbali hasa watoto wetu wa kike na kujikuta wanapoteza ndoto zao,”amesisitiza Prof.Mkenda
Hata hivyo Prof.Mkenda amesema Shule zote zilizohusika katika Udanganyifu wa Mitihani hiyo bado zipo chini ya uangalizi na uchunguzi hivyo ,utakapokamilika hawatasita kuzifutia usajili kwani Wizara ya Elimu haiwezi kuvumilia shule iliyosajiliwa kabisa kugeuka kuwa kiwanda cha udanganyifu.
“Hatutasita wala kuvumilia shule yeyote ambayo imegeuka kiwanda cha wizi na udanganyifu wa mitihani na mbaya zaidi shule hizo zimefanya udanganyifu huo kitaasisi kuonesha kuwa walijipanga kabisa kwa wizi wa mitihani ,hivyo baada ya uchunguzi wote kukamilika hatutamfumbia yeyote macho kuanzia shule zenyewe,wasimamizi mpaka Askari waliohusika nao tutawashughulikia kisheria,”ameeleza Prof.Mkenda.
Aidha, waziri huyo ametoa tahadhari kuelekea mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kuanza Mei 2, 2023 kuwa hawatomvumilia yeyote ambaye atajihusisha na udanganyifu wa namna yeyote kwani udanganyifu wa mitihani haulipi na hautaleta matokeo chanya kwa taifa ambalo linahitaji mafanikio kupitie sekta ya elimu.
Prof.Mkenda amezielekeza Kamati za usimamizi wa mitihani ngazi ya mkoa kuongeza umakini katika usimamizi wa mitihani akitoa msisitizo kwa kamati za usimamizi wa Mitihani mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga ambako matukio mengi ya udanganyifu na wizi wa mitihani wa kidato cha nne 2022 yamejitokeza kwa wingi.