Serikali imejipanga kuongeza ufanisi wa kiutendaji na ukusanyaji wa Mapato wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA kwa kuongeza wafanyakazi na kuboresha makazi ya watumishi, ikiwa ni sehemu ya kutatua changamoto za utekelezaji wa Bajeti ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu wakati wa ziara ya kikazi ya kufuatilia mafanikio na changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Amesema kuwa amebaini upungufu wa takribani wafanyakazi 2000 wa kada mbalimbali katika mamlaka hiyo, hivyo kufifisha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa kiwango toshelevu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Kama Wizara ya Fedha na Mipango tumeona kuna umuhimu wa kuiwezesha TRA katika rasilimali watu na fedha ili kuongeza mapato ya Serikali katika muda mfupi ujao ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla,”amesema Dkt. Kazungu.
Aidha, amesema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi yakiwemo magari, ambapo ameahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kurahisisha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo muhimu katika mstakabali wa ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu TRA, Dkt. Edwin Mhede, amempongeza Dkt. Kazungu kwa kufanya ziara katika Taasisi yake na akamhakikishia kuwa amejipanga kimkakati kuhakikisha mapato yanaongezeka na pia iwapo suala la upungufu wa wafanyakazi litatatuliwa, ongezeko la makusanyo litakuwa sio jambo gumu kwa mamlaka yake.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu, anafanya ziara katika Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Fedha kubaini changamoto za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 na kuangalia utatuzi wake kwa mwaka wa fedha 2019/20.