Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetakiwa kuhakikisha inafufua sekta ya ushirika na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohujumu ushirika na kusababisha machungu kwa wanaushirika ili iwe fundisho kwa wengine.

Akitoa agizo hilo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akifunga maadhimisho ya sherehe za nane nane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika kwenye uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya pia ameitaka Wizara hiyo kupitia upya sekta ya ushirika kwa kuanza na viongozi walipo ndani ya wizara hadi mikoani kuhakikisha kama wanafanya kazi zao ipasavyo na kuwaondoa watakaobainika kwa uzembe.

Waziri Mkuu amesema mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja hawezi kupunguza umaskini bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa nguvu ya kutetea bei ya mazao yao kama ushirika. Aidha, ushirika imara utawasaidia kutafuta soko, kupata mikopo ya riba nafuu.

“Wahimizeni na kuwashawishi wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga  katika vikundi vya ushirika vya uzalishaji na SACCOS. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” Kassim Majaliwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha alisema sekta ya kilimo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mine mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha ziada, ambapo kwa mwaka huu imezalisha kwa asilimia 123.

Ole Nasha alisema katika ukanda wa Nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni nchi mbili tu za Tanzania na Zambia kati ya nchi 15 za jumuia hiyo hazikabiliwiu na baa la njaa.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ladislaus Mwanakatwe naye ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwatetea pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu zilizokuwa zinawakabili wakulima ikiwemo ya tozo.

Mwanakatwe pia ametumia pia nafasi hiyo kuiomba serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo. Pia ameomba Serikali iwezeshe Benki ya Kilimo (TADB) kufungua matawi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili wakulima wake waweze kupata mikopo kwa urahisi.

Jina La Stones Laonekana UEFA Kama Mchezaji Wa Man City
West Ham Utd Wafanya Kweli Kwa Andre Ayew